LIVE MTIZAME HAPA ALIYE CHONGA DILI LA MSUVA
Leo Msuva anatufanulia kwa kiasi kikubwa jinsi ambavyo mmoja kati ya mastaa wa Tanzania walivyomsaidia katika dili lake la kwenda nchini humo.
Msuva anamtaja mchezaji mmoja ambaye kwa kiasi kikubwa kwa roho yake nzuri alisaidia sana dili lake la kwenda Jadida kutoka Yanga kufanikiwa.
Hauwezi kuamini. Ni Elias Maguli, ndiye aliyemuunganishia dili hili. Staa huyo anayecheza naye timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, hakuwa na roho ya korosho kumbania Msuva.
Akiwa ametulia katika kochi lake, Msuva ana kumbukumbu nzuri kuhusu dili hilo na anamshukuru sana Maguli kwa wema mdogo ambao alimtendea ingawa angeweza asiutende kabisa.
“Dili yangu brother ilianzia kwa Jadida kuziona video zangu. Kuna mwakilishi wa klabu yao aliziona video zangu katika Youtube. Walikuwa wanatafuta mchezaji wa aina yangu. Wakamwambia wakala mmoja hivi afuatilie habari zangu,” anasema Msuva.
“Yule wakala akawasiliana na wakala mwenzake ambaye yupo Dubai kuuliza kama ananifahamu. Huyo wakala wa Dubai ndiye ambaye alimuuliza Maguli ambaye wakati huo alikuwa anacheza Oman. Maguli alisema namfahamu ni rafiki yangu ni mchezaji mzuri sana wanaweza kunichukua fasta kama wananihitaji,” anaongeza Msuva.
Kufikia hapo Msuva anatabasamu na kuonyesha kukubali kitendo cha kiungwana cha Maguli. Haitokei mara nyingi sana kwa wanasoka au wanamuziki kupeana dili. Msuva anamshukuru Maguli kwa kupendekeza jina lake bila ya kuweka roho mbaya.
“Angekuwa mtu mwingine angeweza kusema ‘Simjui’ brother. Lakini Maguli alifanya hisani kwa kuniongelea vizuri. Kwani haujawahi kusikia mtu anaulizwa kuhusu mwingine halafu anajifanya hajui chochote? Namshukuru Maguli kwa kweli,” anasema Msuva.
Kuanzia hapo Jadida walianza mchakato wa kumsaka Msuva. Shukrani kubwa kwa mawasiliano ambayo Maguli aliwapa. Baadaye wakawasiliana na Meneja wake, Dk Jonas Tiboroha ambaye alifanikisha dili zima.
Msuva anakiri safari yake kwenda Jadida haikuwa rahisi sana kwa sababu alilazimisha kuondoka. Isingekuwa rahisi kwake Yanga kumruhusu kirahisi wakati ndiye alikuwa kila kitu katika kikosi chao. “Nilimwambia Katibu (Boniface Mkwasa) aniruhusu kwa sababu yalikuwa ni maisha yangu. Mwanzoni Mkwasa alikuwa anasitasita lakini baadaye akawa poa wakakubaliana. Niliwashukuru sana Yanga, wamenikuza wamenilea vizuri lakini ulifika muda wa kuondoka.”
Licha ya uhamisho wake kuibua hisia tofauti kwa mashabiki wa Yanga ambao baadhi yao hawakutaka aondoke kwa sababu alikuwa mchezaji muhimu, huku wengine wakiona ni sawa kwa sababu Taifa linahitaji wachezaji wengi wanaocheza nje, Msuva anaibua siri nzito nyuma yake kuhusu pesa ambazo Yanga walipewa na Jadida.
“Nasikia pesa ambazo Yanga walipewa na Jadida ziliwasaidia kwa sababu walizitumia katika kuwalipa wachezaji mishahara na wengine ambao walikuwa hawajasaini mikataba mipya. Hivyo nashukuru mchango wangu waliuona ndani na nje ya uwanja,” anasema Msuva.
Msuva anakiri maisha mapya ya Jadida yalikuwa yanamtia hofu kwa kiasi kikubwa, huku akiwa hajiamini kama angefanikiwa. Alipatiwa ‘apartment’ ya kifahari anayoishi mpaka sasa ambayo inalipiwa na klabu ya Jadida.
Unalazimika kuchukua lifti na kupanda mpaka ghorofa ya pili katika apartment zao kwa ajili ya kufika kwa Msuva. Kabla ya hapo unalazimika kukutana na walinzi getini na kisha utaulizwa ni wapi unapokwenda.
“Kuna vitu vidogo vidogo ambavyo mimi nalipia wao wanalipa kodi, huku mimi nikiwa nalipia vitu vidogo vidogo ambavyo ni vya kawaida tu. Nalipia mtu wa usafi, nalipia watu wanaokuja kuokota takataka na vitu vidogo vidogo,” anasema Msuva.
Katika eneo hilo sio yeye tu ambaye anaishi katika apartment hizo. Baadhi ya wachezaji wa Jadida wanaishi katika eneo hilo. Mmojawapo ni beki wa kushoto wa Cameroon, Fabrice Ngah ....Soma habari hii kwa undani kwenye Gazeti lako la Mwanaspoti leo Jumapili.
No comments