SIMBA YANGA ZINATAKIWA KUPAMBANA ILI KUSONGA MBELE
TIMU za Tanzania, Yanga na Simba kesho Jumamosi zitakuwa katika hekaheka za kufa na kupona kusaka tiketi ya kusonga mbele katika michuano ya klabu Afrika. Yanga kwa upande wao wapo jijini Gaborone, Botswana na wametua huko kuvaana na Township Rollers kuwania kusonga mbele kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika. Katika mchezo wa kwanza, Yanga inayonolewa na kocha, George Lwandamina ilipoteza nyumbani kwa kuchapwa mabao 2-1.
Simba kwa upande wao wapo nchini Misri wakiwa tayari kwa kupambana vikali na kikosi cha Al Masry katika michuano ya Kombe la Shirikisho.
Katika mchezo wa kwanza, Simba ilipambana na kutoka sare ya mabao 2-2 kwenye mchezo uliokuwa na matukio ikiwemo mvua kubwa iliyosababisha mchezo kusimama kwa dakika kadhaa.
Kwa wale walioshuhudia mechi hizo mbili, watakubali kwamba ilikuwa si michezo ya kudharau hata kidogo, zilikuwa mechi ngumu na zinahitajika mbinu za ziada na kujitolea kwa uwezo wote ili kwenda katika hatua zinazofuata.
Mechi ya Yanga kwa upande wao walikuwa na koswakoswa kadhaa na hivyo, kufanya mashabiki wajiulize kama kweli wanaweza kusonga mbele.
Upande wa Simba ilishuhudiwa mechi iliyokuwa na ushindani kwa pande zote ingawa baadaye mvua kubwa ilitibua huku umeme ukikatika hivyo, kusimisha mchezo kwa dakika kadhaa.
Hata hivyo, baadaye mchezo uliendelea na kumalizika kwa matokeo kubaki 2-2.
Shughuli hiyo, haikuwa ndogo na inamaanisha kwamba, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga wana kazi ngumu mbele yao huku Simba nayo ikiwa katika hali kama hiyo. Lakini, kikubwa cha kufahamu ni kwamba timu hizo bado zina nafasi ya kupambana ndani ya dakika 90 na kubadili matokeo ili kusonga mbele. Na ili kufikia mafanikio, timu zote mbili zinatakiwa kuwa makini katika kila jambo ikiwa ni pamoja na wachezaji kusikiliza maelekezo ya mwalimu na kuyafanyia kazi.
Viongozi wa Yanga baada ya mechi ya awali, waliweka wazi baadhi ya mapungufu yao na kubwa likiwa ni safu ya ulinzi. Kocha Lwandamina na wasaidizi wake walibainisha kwamba, wamefanyia kazi makosa hayo kabla ya kusafiri na kuwa kila kitu kiko sawa. Sasa ni kazi ya wachezaji kuzingatia hayo.
Simba kwa upande wao chini ya kocha, Piere Lechantre ilieleza kuwa wanakwenda kushambulia na pia kujilinda kwani, safu ya ulinzi ilikuwa na matatizo katika mechi ya kwanza. Pia ni kazi ya wachezaji kufanyia kazi maagizo. Mbinu za makocha hao pia ziliungwa mkono na makocha wasaidizi, huku wachezaji wao pia wakisema hakuna haja ya mashabiki wao kuwa na hofu. Pamoja na matumaini hayo, kuna ukweli mgumu ambao mashabiki na Watanzania kwa ujumla wanatakiwa kufahamu, kwamba mechi zitakuwa ngumu na jitihada za makusudi pekee ndio zinaweza kututoa kimasomaso.
Kuna mbinu nyingi za mafanikio, ukiachilia mbali kuzingatia mafuzo ya makocha, pia kuna kukabiliana na changamoto ambazo zinaweza kutokea kabla ya mechi.
Kwa mfano wapenzi wengi wa soka wamekuwa wakiingalia Simba moja kwa moja kutokana na historia ya Waarabu ya kuwa tayari ‘kufia’ uwanjani wakiwa na lengo moja la kuhakikisha wanapiga hatua katika mashindano. Simba wanatakiwa kuwa makini kuhakikisha wanakuwa na utimamu wa mwili na akili kabla ya kupambana na timu hiyo ya Misri
Kwa upande wa Yanga, wao wanaonekana kuwa katika ‘mikono salama’, ingawa ukweli ni kwamba hakuna timu ambayo ingependa kufungwa ikiwa nyumbani au kupoteza nafasi ya kupata fedha. Mawazo ya usalama wa Yanga yanatokana na ukweli kwamba timu za Tanzania zimekuwa hazikumbani na changamoto nyingi wakati zinapokutana na vikosi vya chini ya Jangwa la Sahara.
Lakini, hiyo isiwafanye Yanga wakajiachia na kujiona wako sawa, wanatakiwa kujilinda na changamoto zote ili kuhakikisha kwamba wanakuwa na utimamu wa mwili na akili katika kupambana mpaka hatua ya mwisho. Kuwa na ari ni jambo la msingi katika mafanikio. Kikosi kikiwa na malengo na kikaongezea ari basi ni wazi kwamba kinaweza kufanya vizuri.
Tunazitakia kila la kheri timu zote kufanya vyema katika mechi zao na kuleta heshima kwa Watanzania.
No comments