YANGA SIMBA ZASHTUKIA MCHEZO CAF
YANGA SIMBA ZASHTUKIA MCHEZO CAF?
Klabu hizo kongwe nchini hazina rekodi nzuri kila zinaposhiriki katika mashindano ya kimataifa
In the headlines Yanga, Simba washitukia mchezo CAF
WEDNESDAY MARCH 14 2018
By Imani Makongoro, Eliya Solomon, mwananchipapers@mwananchi.co.tz
Dar es Salaam. Miamba ya soka Yanga na Simba inapitia katika kipindi kigumu katika mashindano ya kimataifa itakapoteremka kwenye viwanja tofauti ugenini kusaka ushindi.
Ni wiki ngumu kwa timu hizo kwa kuwa zinacheza mechi zao za marudiano katika mazingira magumu baada ya kushindwa kupata ushindi katika michezo yao ya nyumbani.
Wakati Yanga ilicharazwa mabao 2-1 dhidi ya Township Rollers ya Botswana, Simba ililazimishwa sare ya 2-2 na Al Masry ya Misri.
Yanga wanahitaji ushindi wa kuanzia mabao 2-0 au zaidi ili kuingia katika hatua makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Vinara wa Ligi Kuu, Simba inatakiwa kupata ushindi wowote ili kusonga mbele katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mechi zote mbili ni ngumu kwa timu hizo kwa kuwa zinakwenda kucheza ugenini kwa presha kubwa baada ya kushindwa kuwa na mtaji mzuri wa mabao ya nyumbani.
Kocha Mkuu wa Yanga, Mzambia George Lwandamina alisema mchezo utakuwa mgumu, lakini ana mbinu za kupata ushindi.
Lwandamina alisema anakwenda Botswana kucheza soka ya kushambulia kwa kasi ili kupata mabao ya mapema yanayoweza kuwavuruga wapinzani wao.
Kocha huyo alisema amejiandaa kwa mbinu tofauti za kupata ushindi ikiwemo kucheza kwa kufanya mashambulizi mfululizo huku ikijilinda vyema katika safu ya ulinzi.
“Siwezi kusema kila kitu kuhusu mbinu zangu, mimi ni kocha zingine zitabaki ndani ya nafsi yangu, lakini kikubwa tunakwenda kucheza soka ya kushambulia huku tukichukua tahadhari ya kujilinda,” alisema Lwandamina.
Kocha huyo wa zamani wa Zesco ya Zambia, anatarajiwa kutumia mfumo 4-4-2 ambao unatoa fursa kwa timu kucheza kwa kushambulia zaidi.
Wachezaji kujazwa mapesa
Klabu ya Yanga imesisitiza kuwa itawatendea haki wachezaji wake endapo watajituma na kuitupa nje Rollers katika mchezo wa Jumamosi.
Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa alisema klabu hiyo imetenga donge nono kwa wachezaji wao ikiwa ni sehemu ya motisha.
“Tutawapa motisha wachezaji wetu kama wataitoa Township ni lazima, kiasi gani tutawapa hayo ni masuala ya ndani,”alisisitiza Mkwasa.
Yamegewa siri kuiua Rollers
Mshambuliaji wa Tanzania, Rashidi Mandawa anayecheza soka ya kulipwa katika klabu ya BDF XI ya Botswana, alisema njia pekee ya Yanga kupata ushindi ni kufanya mashambulizi ya kushitukiza.
“Yanga inatakiwa kufanya mashambulizi ya kushitukiza, isithubutu kucheza mchezo wa kufunguka ni hatari kwa sababu hawa jamaa ni hodari,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar.
“Pia wajiandae kisaikolojia kwa sababu Botswana nzima ni Township Rollers, linapokuja suala la mechi za kimataifa watu wote hapa wanaungana,”alisema Mandawa.
Simba yashitukia fitna Misri
Simba inatarajiwa kuondoka leo mchana baada ya kumaliza mazoezi asubuhi, lakini vigogo wa klabu hiyo wamesema wamejipanga kukabiliana na fitna za Waarabu.
Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema watatibua kila fitna itakayoelekezwa mbele yao na wenyeji kabla ya kuivaa Al Masry Jumamosi kwenye Uwanja wa Port Said.
“Tumejiandaa kwa kila kitu, timu yetu iko vizuri na uongozi tumejipanga, tunazijua fitina za Waarabu, tumejiandaa kuzipangua,” alisisitiza Abdallah.
Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma alidai hawezi kuweka hadharani mbinu za kuing’oa Al Masry ingawa alisisitiza wamebaini udhaifu wa Waarabu.
“Tunakwenda kucheza ‘game’ ngumu lakini tunajua Waarabu watakamia, sisi tumejiandaa kimwili na kiakili kwa ajili ya kushinda, tunachohitaji ni bao la mapema na ushindi tu,” alisisitiza Djuma.
Wasikie Chambua, Costa
Nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Sekilojo Chambua alisema Yanga inatakiwa kusahau kama ilipoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Rollers.
“Matokeo ya kupoteza nyumbani sio mazuri, lakini Yanga inatakiwa kwenda na mtazamo chanya, wajione kama kazi inakwenda kuanza upya kule, bado naona wanaweza kupata ushindi, mpira hauna cha ugenini,”alisema Chambua.
Beki wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Victor Costa alisema timu hizo zinakabiliwa na mechi ngumu lakini wachezaji wamebeba dhamana ya kuwakomboa Watanzania.
Libero huyo alisema kuwa wachezaji wa Simba na Yanga wanatakiwa kujitoa kwa nguvu zote kupata ushindi.
No comments