Kocha simba afunguka sababu kumtosa kapombe dhidi ya gendarmerie
Shomari Kapombe amerejea katika kiwango chake, baada ya kucheza mechi tano kali mfululizo zikiwemo za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Beki huyo wa kulia, alikuwa majeruhi yaliyomuweka nje ya uwanja kwa miezi sita kabla ya kurejea kwa kishindo kwenye mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kapombe aliyerejea Simba kutoka Azam, amekuwa kivutio kwa mashabiki wa Simba na wamemsahau Hassan Kessy aliyetimkia Yanga. Kutokana na ubora wake, baadhi ya mashabiki hawakutarajia kumuona Kapombe akiwa jukwaani dhidi ya Gendarmerie.
Kocha Pierre Lechantre amevunja ukimya baada ya kueleza sababu ya kumuacha benchi mchezaji huyo katika mchezo huo. Lechantre amesema aliamua kumuweka benchi Kapombe kwa kuwa amechoka, baada ya kucheza mechi nyingi mfululizo.
“Niliongea naye kabla ya mchezo, nikamwambia umechoka, umetoka kwenye majeruhi na umecheza mechi tano ngumu mfululizo, hivyo umechoka,” alisema Lechantre.
Kocha huyo alisema Kapombe anatakiwa kupumzika ili kupata muda mzuri wa kujiandaa na mashindano ya Ligi Kuu na mechi ijayo dhidi ya Al Masry ya Misri.
No comments