BREAK NEWS

TULIENI MUONE MAMBO YA SIMBA JUMATANO



SIMBA ipo kwenye maandalizi ya mwisho kabla ya kuvaana na Al Masry ya Misri iliyotua kimyakimya alfajiri ya jana, katika mechi ya Kombe la Shirikisho la Afrika, huku benchi la ufundi la Msimbazi likiwatuliza mashabiki wao.
Benchi hilo limesema hakuna haja ya mashabiki kupaniki kuelekea mchezo huo wa keshokutwa Jumatano kwani, wanajua wanacheza na timu ya aina gani na tayari mafaili ya nyota wa Misri yapo mikononi mwao na watawanyoosha Taifa.
Simba na Al Masry iliyotoka kupata ushindi wa mabao 3-1 katika Ligi Kuu ya kwao, zitavaana Jumatano saa 12:00 jioni katika mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma alisema, licha ya kuwa na majukumu yao ya mechi za Ligi Kuu Bara, lakini walikuwa wakiwafuatilia kwa karibu wapinzani wao hao na kwamba wameshanasa mbinu zote za nyota wao.
Al Masry ina nyota wanaowatia matumbo joto mashabiki wa Simba akiwamo Ahmed Shoukry, Aristide Bance, Ahmed Gomaa, Islam Salah na wengine, lakini Kocha Djuma alisema Simba haina sababu ya kuwa na presha na mchezo huo.
MSIKIE
Akimchambua Bance, Djuma alisema; “Tunajua ni mshambuliaji hatari ambaye ana uwezo wa mkubwa wa matumizi ya nguvu pindi anapokuwa anamiliki mpira, mzuri katika kufunga na anaweza kufunga mipira ya juu kwani anaweza kupiga mipira ya vichwa.”
“Ila si mzuri katika mbinu kwani kuna watu wanafanya kazi ya kutafuta mipira na kumpasia yeye ambaye muda mwingi hachezi mbali na eneo la goli la wapinzani na tumeshaliona hilo na tunalifanyia kazi kwa wachezaji wetu,”
“Tutakuwa makini katika timu yetu kumkaba dhidi yake na mabeki wetu watakuwa wa kwanza kuokoa mipira yote ambayo atakuwa anapasiwa na tukiweza kufanya hivyo kwa umakini zaidi itakuwa rahisi kwetu kumzuia.”
GOMAA JE?
Kuhusu Ahmed Gomaa, Djuma alimchambua kwa kusema: “Ana uwezo mzuri katika kufunga tena anacheza vizuri kwa maelewano na wenzake na anauwezo pia wa kimbinu anachezea mpira na kwetu hatutamuacha huru kupokea mipira mara kwa mara.”
“Gomaa ana uwezo pia wa kuwatengenezea nafasi wenzake kama atashindwa kupata nafasi ya kufunga na si mzuri katika matumizi ya nguvu kama ilivyokuwa kwa Bance na kama akipata nafasi moja tu anaweza kutumia na kufunga,”
“Anaweza kumiliki na kuchezea mpira zaidi hilo tumeliona na sidhani kama atakuwa anapata nafasi kama hiyo kwa maandalizi ambayo tumefanya tutamzuia ili asilete madhara kwetu kwani ni mojan ya mchezaji nyota wa kikosi hiko,”
NYOTA WENGINE
“Gomaa na Bance tumewaona na tunazo taarifa zao lakini hata timu yao tumeiangalia na tumewaona wachezaji wote jinsi na wanavyocheza na tunatarifa zao za kutosha ambazo tunazifanyia kazi kabla ya mechi yetu,” alisema Djuma.
“Wanacheza kitimu kwani wakiwa wanakaba wanaka wote lakini hata wakiwa wanashambulia wafanya hivyo, lakini tumeona kuwa wakicheza ugenini wanakuwa waoga kushambulia mara kwa mara basi sisi tutatumia nafasi hiyo kupata matokeo ya ushindi ingawa haitakuwa rahisi,”
MIPANGO KAMAMBE
Kocha Djuma alifichua walivyojiandaa na mchezo huo akisema: “Tutacheza kinyumbani zaidi kwa kushambulia ili kupata mabao ya haraka na ya kutosha ili iwe salama kwetu kwa mechi inayofaata ambayo tutacheza ugenini kwani mashindano haya muda mwingine matokeo ya nyumbani ni muhimu mno.”
“Katika kukaba tutacheza mfumo wetu wa kukaba kuanzia wachezaji wa mbele ili kuanza kupunguza mashambulizi ambayo yanaweza kuwa ya hatari kwa upande wetu na muda mwingi tunataka kuwa salama,”
“Tutajitahidi kupunguza makosa ambayo tunafanya mara kwa mara kwani kucheza na timu iliyokuwa na wachezaji wazoefu wa mashindano kama haya hautakiwi kufanya jambo kama hilo zaidi ya kuwa makini katika kukaba na kutumia nafasi katika kushambulia,”
“Tutaingia katika mechi hii kwa kuwaheshimu Al Masry kwani ni timu yenye uzoefu katika mashindano haya na hata wachezaji wao ni wazoefu pia na nidhamu hiyo inaweza kuwa sababu kwetu ya kuwafunga na kupata matokeo ya kusonga mbele,” alisema Kocha Djuma anayemsaidiana na Pierre Lechantre kutoka Ufaransa.

No comments